Na: Bujaga Izengo Kadago- Ofisi ya Mawasiliano na Masoko SUA

Changamoto imetolewa kwa wadau wa mafunzo ya kilimo katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara kutafuta ufumbuzi wa     nchi hizo kuendelea kukabiliwa na hali tete ya usalama wa chakula ili hali nchi hizo zina ardhi ya kutosha yenye rutuba, maji ya kutosha na nguvu kazi ya vijana.

 

Changamoto hiyo imetolewa na Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Raphael Chibunda alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu inayojadili namna bora za kujengea uwezo wanafunzi wa masomo ya sayansi katika kilimo miongoni mwa vyuo vikuu vya kilimo barani Afrika, warsha inayofanyika SUA mkoani Morogoro.

 

 

Prof. Chibunda amesema warsha hiyo haina budi kutafuta majibu kwanini hadi leo waafrika siku inapita bila mlo wa uhakika, wakulima wetu wangali wanalima kilimo cha mababu zetu, mamilioni ya watoto chini ya miaka mitano wanapoteza maisha kutokana na kukosa lishe sahihi katika milo yao, nchi za Afrika zinaendelea kuagiza mamilioni ya tani za chakula kutoka nje ya bara letu.

 

Aidha Prof. Chibunda amesema bara la Afrika lina neema ya maji kwani maji yanatiririka na kupotelea baharini kama vile hakuna wataalamu wa teknolojia ya umwagiliaji katika nchi zetu, na mamilioni ya mazao ya kilimo yanapotea wakati wa uvunaji mazao hayo kutokana na matumizi hafifu ya teknolojia sahii za uvunaji mazao.

 

Kutokana na changamoto hizo Makamu waMkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sua amewataka wahadhiri hao wa kilimo kutoka vyuo vikuu vya kilimo barani Afrika na Marekani kutoka na maazimio yatakayopelekea wahitimu vyuo hivyo vikuu barani Afrika kuja na mbinu mpya za ufundishaji na ujasiliamali utakaosaidia kutoa wahitimu watakaojibu changamoto mbalimbali za wakulima vijijini na hivyo kuleta mapinduzi ya kilimo chenye tija kwa wakulima wa mataifa ya Afrika.

 

Prof. Chibunda amesema kama vyuo vikuu barani Afrika vina wajibu wa kutekeleza lengo namba mbili la mkakati wa maendeleo endelevu( SDG) linalolenga katika kuondoa njaa, kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na kuboresha lishe na lishe na lengo namba nne linaungumzia hakikisho la elimu bora na shaihi kwa wote na kwa maisha yao yote, na malengo hayo mawili yatafanikiwa iwapo warsha hiyo itatambua hitaji la sayansi, teknolojia na ubunifu kujumuishwa kwa dhati katika sekta muhimu za maendeleo kama vile kilimo, nishati, mazingira, afya na nyinginezo nyingi.

 

Mapema akizungumzia madhumuni ya warsha hiyo Rasi wa Ndaki ya Kilimo katika chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Frederick Kahimba amesema kushiriki kwa wataalamu kutoka ndaki ya kilimo katika vyuo vikuu barani Afrika kutawawezesha kupatikana uzoefu wa kutosha katika kujengea uwezo ufundishaji na kuboreshwa kwa mitaala ya masomo ili kutoa wahitimu watakao kwenda kutoa majibu sahihi kwa wakulima vijijini na sio wahitimu wanaotafuta ajira pekee.

 

Naye Prof. Tag Demment kutoka chuo Kikuu cha California Marekani alisisitiza haja ya vyuo vikuu vya kilimo barani Afrika kutambua wajibu wao katika kutekeleza agizo la viongozi wa Afrika linalotaka ifikapo mwaka 2030 wataalamu na wakulima wa Afrika wafikie malengo ya kuwa na kilimo endelevu na usalam wa chakula.

 

Pia Prof Demment amewataka washiriki wa warsha hiyo kuja na mpango kazi kwa vyuo vikuu vya kilimo barani Afrika kubuni namna bora ya elimu ya kilimo itakayowanufaisha wadau wa ndani na nje ya vyuo hivyo.

 

 

Save

TOA MAONI YAKO HAPA