Na:Farida Mkongwe

 

Wazee wa kituo cha kulelea wazee wasiojiweza cha fungafunga kilichopo Manispaa ya Morogoro wameishukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira  MORUWASA kwa kuwapelekea huduma ya majisafi na hivyo kuwaondolea kero ya upatikanaji wa maji safi iliyokuwa ikiwakabili.

 

Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake mara baada ya kupokea misaada ya vyakula vya aina mbalimbali vilivyotolewa na MORUWASA mmoja wa wazee hao SAIMON NJEGA amesema kuwa kwa sasa wanafarijika sana kwa kuwa wameweza kuepukana na kero ya kutumia maji ya chumvi, kero ambayo ilikuwa ikiwasumbua hasa kwa upande wa maji ya kunywa.

 

Awali akizungumza na wazee hao mara baada ya kufanya usafi na kuwakabidhi wazee hao misaada hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MORUWASA Injinia NICHOLAUS ANGUMBWIKE amesema wanatambua thamani waliyokuwa nayo wazee hao na ndiyo sababu waliamua kuwapelekea huduma ya maji, kufanya maamuzi ya kwenda kufanya usafi na kutoa misaada ya vyakula katika wiki hii ya maadhimisho ya sherehe za maji.

 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mfawidhi wa kituo hicho cha Fungafunga bw. RASHID OMARY pamoja na kuwashukuru watu mbalimbali wanaojitolea kutoa misaada katika kituo hicho pia ameikumbusha jamii katika ngazi ya familia kuchukua wajibu wao wa kuwalea wazee badala ya kuwatelekeza na kuwaacha wakiangaika ovyo mitaani.

 

Maadhimisho ya sherehe ya wiki ya maji yameanza tarehe 16 mwezi huu kwa MORUWASA kufanya shughuli mbalimbali za uhifadhi wa mazingira ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti na yatafikia kilele tarehe 22 mwezi huku yakibeba kauli mbiu isemayo”Majisafi na majitaka punguza uchafuzi, yatumike kwa ufanis”.

 

 

 

TOA MAONI YAKO HAPA